MABADILIKO NI WEWE 2020

Jeremiah Paul Wandili
4 min readDec 30, 2019

“Be the change that you want to see in the world.”-Mahatma Gandhi

Image source; Crushpixel

Katika kuelekea hitimisho la Kalenda ya Mwaka 2019, ninaguswa kushare nawe jambo moja muhimu kuhusu Mabadiliko. Andiko hili nimeliandaa baada ya kupata chachu kubwa kutoka kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki kuhusiana na namna wanavyochukulia mabadiliko hasa ya Mwaka Mpya.

Kwa kipindi kirefu imezoeleka kuwa “MWAKA MPYA NA MAMBO MAPYA” msemo huu umekuwa sehemu ya kujenga hamasa na imani kubwa kwa watu wengi katika matarajio ya mambo mapya ambayo utarajiwa kuja na Mwaka Mpya. Hivyo si ajabu kwa wengi wetu kuendelea na harakati za kuhitimisha Mwaka 2019, huku tukiwa na matarajio ya mabadiliko kadha wa kadha katika Mwaka 2020.

Change is personal, mabadiliko ni ya mtu binafsi na kamwe mabadiliko ya mtu mwingine hayawezi kuwa yako. Japo kwa namna moja au nyingine ukiwa mtu wa karibu na mtu aliyechukua hatua katika mabadiliko yanaweza kukuathiri kwa namna moja au nyingine. Hivyo tunavyozungumzia nadharia ya mabadiliko tunagusa mtu mmoja mmoja. Na chanzo kikubwa cha mabadiliko ni MAAMUZI. Pale mtu mmoja mmoja anapoamua kufanya maamuzi katika maisha yake (Dunia yake) ndio mabadiliko utokea.

MABADILIKO NI WEWE, unapokuwa na kiu ya kuona mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha yako ni wewe mwenyewe ndio unalojukumu la kufanya maamuzi na kuhakikisha unakuwa badiliko lile unalotarajia kuliona.

Kwa kuwa maisha yana nyanja mbalimbali na vivyo hivyo matamanio katika mabadiliko ni mengi. Ni lazima kuainisha nyanja ambazo binafsi unatazamia kuona mabadiliko. Nyanja za Kijamii, kiuchumi na fedha, familia, mahusiano, elimu, makazi, afya, taaluma, kiroho, na hali ya ustawi kwa ujumla.

Spheres of Life; Picture courtesy

MABADILIKO ni matokeo ya jitihada zinazofanyika baada ya kuchukua maamuzi. Kwa walio wengi wamekua na dhana na mtazamo tofauti dhidi ya nadharia ya mabadiliko. Wengi wamedhani ni mfumo wa Kisiasa na uchumi wa nchi ndio unaoweza kuleta mabadiliko yao binafsi.

Pamoja na kuwa yapo mahusiano ya moja kwa moja katika nadharia ya mabadiliko na misukumo ya kisiasa na kiuchumi ila kwa ujumla wake mabadiliko hayo yanagusa zaidi mifumo ya kijamii na sio mtu mmoja mmoja.

Katika kipindi hichi cha mwisho wa mwaka, kuna dhana pana imeshaanza kujengeka katika swala la kufanya tathmini binafsi kuhusu maisha kwa ujumla na namna ambavyo malengo yameweza kufikiwa. Msingi wa kufanya tathmini ni mzuri sana na unaleta hamasa zaidi katika kuwezesha maisha kuwa ya mvuto zaidi.

Mabadiliko binafsi uhusisha nyanja katika maisha ya mtu mmoja mmoja. Hivyo wakati wa kupanga malengo ya Mwaka Mpya (2020) kama ilivyokuwa kwa Mwaka 2019, kuna kuwa na vipaumbele katika kila nyanja za Maisha. Kwa mfano; Unaweza kutazamia mabadiliko katika nyanja ya Mahusiano na Familia, hivyo ni lazima kuainisha vipaumbele katika nyanja husika ili kurahisisha kupanga malengo kwa uSMART.

Yaweza kuwa moja ya lengo lako na sehemu unayotarajia kuona mabadiliko ni kuongeza ujuzi katika taaluma yako, hivyo ni lazima vipaumbele viandaliwe kulingana na nyanja husika na maamuzi yafanyike ili kuruhusu kuchukua hatua katika kuliendea lengo husika. Zaidi, ikumbukwe mabadiliko ni gharama na lazima kuilipa ili kuweza kuona mabadiliko.

Socialization

Hakuna mabadiliko bila kulipa gharama. Ni lazima kutambua gharama zinazohitajika katika kufikia mabadiliko tarajiwa. Yaweza kuwa moja ya nyanja unayoitazamia kuona mabadiliko ni swala la zima la Afya. Na katika kuifikia afya bora, itakulazima kubadilisha aina ya vyakula, muda na pia kuzingatia mazoezi. Hivyo kuna gharama kubwa utahitajika kuilipia ili kufikia mabadiliko stahiki.

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA KUWA MABADILIKO UYATAKAYO;

Yapo mambo kadhaa lazima kuyazingatia ili kufikia mabadiliko;

  1. Kuwa tayari kulipa gharama, kama nilivyotoa utangulizi hapo juu, mabadiliko yanahitaji kulipa gharama, kwa mfano; Muda utakaohitajika wa ziada katika kufanya mazoezi, au muda wa ziada katika kuamka mapema zaidi ili kujisomea au kuchelewa kulala ili kushiriki mazoezi n.k.
  2. Kuchangua marafiki na kujenga mahusiano. Kwa namna moja au nyingine, mabadiliko unayotarajia yatahitaji wewe binafsi kuimarisha mahusiano na marafiki wapya au mtandao wako wa marafiki.
  3. Kukubali kupoteza baadhi ya marafiki, lazima ukubali kuwa moja ya gharama ya kufanya uchaguzi kufikia mabadiliko ni kuwapoteza baadhi ya marafiki ambao kwa namna moja au nyingine mabadiliko unayotarajia na hatua unazochukua zitawagusa hivyo kuwapoteza kabisa.
  4. Kufanya maamuzi, ilikuyafikia mabadiliko unayotarajia lazima uwe tayari kufanya maamuzi na kuyaheshimu. Kama itakubidi kubadili aina ya chakula, kubadili muda, kujifunza lugha, kuanza kozi mpya au hata kulipa fedha kwa ajili ya kuhudhuria semina n.k
  5. Wekaza muda kujifunza mbinu mpya, ili kuyafikia mabadiliko tarajiwa, ni lazima kutafuta maarifa, ujuzi na mbinu mpya zitakazo kuwezesha kuyafikia mabadiliko kwa mafanikio zaidi. Hauwezi kufanya mambo yale yale, kwa namna zile zile huku ukitegemea matokeo tofauti. Ni lazima utafute mbinu, ujuzi na maarifa mapya kuelekea mabadiliko tarajiwa.

Kwa kuhitimisha, katika mzunguko wa maisha ya mwanadamu, ni uchaguzi katika kufanya maamuzi ndio unaoleta matokeo na sio nadharia na tafakari pekee. Hata ukipewe siku 365 za Mwaka 2019 tena, kama hautofanya maamuzi, hautochagua na kubaki unatarajia matokeo hautoona mabadiliko. NOTHING WILL CHANGE UNLESS YOU DO.

--

--

Jeremiah Paul Wandili

| Community Development | BDSPM Consultant| YALI Alumni, Founder & Executive Director @woteinitiative Youth Leadership Advisory Board, Member #YLAB @DOTTanzania