MAMBO NI MENGI…..MUDA MCHACHE

Jeremiah Paul Wandili
7 min readDec 31, 2019
Picha kwa hisani ya Mtandao wa Google.

Ikiwa ndio kwanza Mwanzo wa Mwaka Mpya wa 2020, nichukue fursa hii kukupongeza na kukutakia kila lenye heri katika mafanikio ya Mwaka Mpya. Yaweza kuwa Mwaka ni mpya ila mambo ni yale yale (Yale Yale). Najua upo na ratiba nyingi sana, na pia hamasa kubwa Zaidi katika kuanza Mwaka Mpya. Najua pia upo katika pilikapilika za kuanza Safari kurudi katika sehemu za Kazi baada ya Likizo ya Siku Kadhaa kutokea Sikuu ya Noeli.

Tayari Mwezi Januari una mambo mengi, safari nyingi na majukumu mengi…. Mwezi ambao umepewa majina mengi…Unaitwa Tatu bomba, unaitwa Njanuari, unaitwa Two in one…. Basi yote ni katika kuonyeshe inavyokuwa changamoto katika kukabiliana na mahitaji makubwa ya shughuli za Januari.

Kitu kikubwa cha Muhimu ni kuwa Siku 31 za Mwezi Januari hazijawahi kuongezeka. Mahitaji katika mwezi Januari yanaweza kuwa yanaongezeka kila Mwaka inategemea na mtu mmoja na mwingine. Mwisho wa siku, mwezi wa Februari nao uwa unaamua kuchukua nafasi…ila napenda uvute pumzi, unapouanza Mwaka Mpya, ANZA NA MUNGU katika kila jambo…..

Nimepata nafasi kufuatilia kwa ukaribu mambo mbalimbali katika jamii na kujifunza mambo mengi sana, utakumbuka ni juzi tu nilishare nawe mambo kadhaa kuhusu mabadiliko na Msisitizo ulikuwa “MABADILIKO NI WEWE” na wengi wa wasomaji mmenitumia ujumbe kuchangia katika andiko lile na Zaidi mmenipongeza katika kushare nanyi maarifa kadhaa. Nami ninashukuru sana kwa mrejesho na nitaendelea kushare nanyi kadri Mungu atakavyotupatia nafasi na fursa.

Picha kwa hisani ya Mtandao wa Financial Times

Sitopenda sana kuchukua muda wako mwingi katika kuandika maneno mengi sana najua tayari ndugu msomaji mambo yako ni mengi na muda ni mchache. Najua wale waliosema 2020 nitafanya hiki na kile tayari wapo mbioni kufanya, yule anayepanua biashara, anayehamisha eneo la biashara na wengine ambao wapo mbioni kuelekea BRELA, TRA, SIDO TMDA na sehemu zote zinazohusiana na urasimishaji biashara, yote hiyo ni kuhakikisha Maisha yanaendela na malengo yanatimia. Ili kuhakikisha ufanisi na umakini mkubwa katika kutekeleza malengo ya Mwaka 2020, ninapendekeza kwako, BADILIKO Muhimu sana katika kutunza na kuutumia MUDA kwa manufaa yako.

Mwaka 2019 umekuwa ni Mwaka wa Baraka kubwa sana na rehema za Mungu wetu zimetuvusha wote salama najua wengi wa wapendwa wetu hatukonao leo na wengine hawako vizuri Kiafya ila sisi tunaopata nafasi kujumuika hapa ni ishara ya upendeleo mkubwa ambao Mungu wetu ametukrimia.

Hakuna namna nzuri ya kulipa fadhila za Mungu wetu, maana hata uhai huu hakuna anayestahili, pumzi tunayoivuta hakuna anayeilipia, sote tu sawa mbele zake na sote ni watoto wake wapendwa. Hivyo ni jukumu langu na lako pia kuhakikisha tunaifanya dunia kuwa sehemu salama na bora Zaidi ya tulivyoikuta na Zaidi ya tutakavyoiacha.

Je wajua, leo kuna biashara mpya mamilioni zinazaliwa, mawazo mabilioni yanabuniwa na Zaidi ya yote kutokana na ukuaji wa Sayansi na Teknolojia changamoto mpya zinaongezeka. Katika kasi ya ukuaji wa Teknolojia, ubunifu unazidi kuongezeka, maarifa yanaongezeka na aina nyingi za kuongeza ufanisi zinaongezeka. Kitu muhimu ninapenda kukushirikisha ni wewe tu kuamua kufikiria tofauti, usikubali kufuata mkumbo…ule wa MAMBO NI MENGI MUDA MCHACHE, lazima uwe makini katika kupangilia mambo yako, kuutawala muda wako na kujiwekea vipaumbele ambavyo vitakusaidia kutumia muda kwa manufaa Zaidi katika kufikisha malengo yako sehemu stahiki ya mafanikio.

Fikiria ni kwa namna gani MAMBO NI MENGI NA MUDA NI MCHACHE, kauli hii imejizolea umaarufu mkubwa sana katika kipindi cha Mwaka 2019, kutokana na matukio mbalimbali yanayojitokeza katika mitandao ya kijamii. Mitandao ya kijamii imeikuza sana kauli hii na pia imepelekea Mambo kuwa Mengi na kweli muda umekuwa finyu sana.

Najua inakuwia vigumu kuacha matumizi ya mitandao ya kijamii, najua ilivyongumu kukaa mbali na MTANDAO, unaweza pata homa ya ghafla, mambo yakikupita unajihisi kama umekosa mambo ya msingi sana. Ila kwa Mwaka 2020, lazima nawe uwe mjanja (BE SMART) unavyotumia Simu Janja yako zile selfie za kibabe ukiwa umedamshi kweli zikose kukaa kwa STATUS ahaha hapana. Lazima ujue mbinu za kijanja kubalance na kutumia Muda katika ulimwengu huu wa kijanja.

Kuna mambo kadhaa nimekuandalia ili ukae mkao wa kijanja katika kuwa na MAMBO MENGI KATIKA MUDA MWINGI, wewe kwanini muda wako uwe mchache? Muda ni Mali, Muda ni Pesa..je ungetamani uwe na Pesa chache huku majukumu yako yawe mengi?? Hapana lazima muda/mali/pesa ziwe za kutosha ili kukamilisha mambo mengi.

Katika zama hizi za ukuaji wa Sayansi na Teknolojia. Yapo mambo yanayoweza kupelekea ukatumia muda wako kwa hasara au kwa faida; Fursa hii ninakushirikisha mambo kadhaa ambayo unapaswa kuyacheki kijanja ili matumizi yake yasiwe ya Hasara kwako.

  1. Matumizi ya Mitandao ya Kijamii

Mitandao ya Kijamii (Facebook, Twitter, Insta, Telegram, Whatsup n.k) inapotumika vizuri inafaida kubwa sana na pale inapotumika pasipo uangalifu inaleta hasara kubwa na kupelekea Mambo yako yakawa mengi na muda ukawa mchache. Kadri unavyotumia mitandao ya kijamii kama genge au kijiwe utakumbana na taarifa mbalimbali na matukio ambao yatapelekea muda wako kupotea haraka sana.

Picha ikionyesha mpango wa Kalenda kwa hisani ya Excel

Kila mmoja wetu leo hii tunazo siku 365 kama akiba yetu, chukulia muda wako kama rasilimali muhimu au mtaji wako, je ungependa kuutumia kushinda Youtube kuangalia vichekesho, hapo hapo uchungulie page zote kule Insta, ukitoka hapo uingie Twitter, kisha ucheki na Facebook,Vipi Magroup ya Whatsup ahaha… hapo hapo Status zako katika Whatsup haujafuatilia nani aliyeview….ahaha Muda lazima uwe mchache. Maana kila sekunde kuna habari mpya au picha mpya, au video mpya inawekwa nawe kwakuwa hautaki kupitwa unajikuta umetumia Masaa matatu kwa siku au Zaidi kufuatilia na kusoma matukio mbalimbali….

2. Mazungumzo ya muda mrefu kwa njia ya simu (kuongea au kuchat kwa sms)

Aisee, kuna watu wanajua kutumia dakika zao za ofa, au sms zao na wengi pia wanajikuta nao wanashindwa kukatisha mazungumzo hivyo, kupelekea muda mwingi kutumia katika mazungumzo. Hii inatokea kwa walio katika sehemu za Kazi, Wajasiriamali wakubwa na wadogo na hata wale walio nje ya mfumo wa ajira au biashara. Kikubwa hapa ni muda unaotumika katika mazungumzo hayo na mchango wa mazungumzo hayo katika kuyafikia malengo au vipaumbele katika siku husika. Ni muhimu kufanya mawasiliano lakini ni muhimu Zaidi kuzingatia muda katika kufanya mawasiliano.

Kuna watu wanawahi makazini ila akifika kazini anajikuta muda mwingi unatumika katika mazungumzo na kusahahu hata sehemu kubwa ya majukumu. Najua yapo mashirika na taasisi yanayozuia matumizi ya simu wakati wa kazi. Ila muhimu mtu mmoja mmoja kuanza kujenga utamaduni wa kuheshimu muda.

3. Foleni katika kupata huduma au wakati wa usafiri, katika benki na sehemu nyingine za huduma za kijamii.

Muda mwingi umepotelea katika changamoto za foleni na kusababisha kupungua kwa ufanisi na umakini kwa mtu mmoja mmoja au taasisi. Ikiwa ni mwanzo wa Mwaka, lazima kujifunza mbinu za kuepuka foleni pale itakapobidi kuwahi mapema na kukadilia muda katika njia ambazo foleni zake zinafahamika ili kuhakikisha muda unatumika vizuri. Lakini inapobidi, kufanyia kazi nyumbani. Swala la foleni ni changamoto kubwa, ila muda mwingine mtu anajikuta katika foleni pasipo ulazima.

Picha ikionyesha eneo la Soko la Kariakoo kwa hisani ya Brainbongo

Kwa mfano unakwenda kupanga foleni Benki kulipia karo au huduma mablimbali, ilihali kuna njia nyingine rahisi na salama katika kufanya mihamala kwa njia ya simu ya mkononi au mawakala. Muda mwingine kutumia huduma za usambazaji katika kuhakisha gharama inakuwa na tija na muda unaotumika unakuwa wa faida..utajikuta inakubidi uende Kariakoo, wakati itakulazimu kwenda na kurudi, kukutana na foleni nyakati zote ilihali ungeweza kutumia mifumo au huduma za usambazaji (Delivery services).

4. Marafiki au watu wengine tunaokuwa na mihadi nao.

Wakati mwingine kwa kuwa watu wengi bado hawajazoea kutunza muda na kuheshimu muda wamekuwa wakichangia katika kuleta hasara ya muda wa wengine. Wakati mwingine kughairisha mihadi wakati wa muda husika. Hii yote inachangia kuleta hasara katika matumizi ya muda. Hivyo hii ni changamoto kubwa sana pale ambapo umehudhuria katika kikao au mkutano uliopangwa kufanyika kwa mfano; Saa 2:30 asubuhi ila unakuta wahusika wanafika katika kikao saa 4 kasoro. Mara kwa mara maswala ya utunzaji wa muda imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kwa vile wengi wetu hatuthamini muda kutokana na mazoea.

Katika Mwaka 2020, kuwa mabadiliko uyatakayo kuyaona na hasa heshimu muda, utunze muda na tumia kwa mafuaa ya malengo yako. Pale inapobidi jiepushe na makundi ya marafiki wanaopenda kuishi kwa mazoea na hasa wale ambao wanaishi katika kanuni ya Nipo hapa Napoteza poteza muda.

Hawa ndio wale wanaoweza kukupigia simu na kuongea kwa muda mrefu, mazungumzo yasiyo na tija. Hawa ndio wale pia wanaoshare picha za ajali na matukio mengine utadhani wanalengo la kusaidia waathirika au kuhamasisha uokoaji.

Mwaka 2020, wewe ni mabadiliko na mabadiliko ni wewe…kubali kulipa gharama, usikubali kuwa mmoja wao..usiwe wale wa MAMBO NI MENGI MUDA MCHACHE, wale ambao wanashare taarifa zenye taharuki, wale wanaoscreenshot twiti za taarifa za kuleta hofu na taharuki kutoka Twita. Usikubali kuwa kama wale wanaokubali kupoteza muda.

Unapopoteza muda unakuwa umekubali kupoteza mtaji wako. Maana moja ya rasilimali muhimu tunayopewa wanadamu bure kabisa ni MUDA. Muda ni mali yako, muda ukiutumia vizuri utakuwa ni Asset (Faida) na utakapo utumia vibaya utakuwa ni Liability (Hasara). Wewe ndio mwenye kufanya uchaguzi na maamuzi namna utakavyo utumia muda wako.

Ni kweli Muda Mchache na Mambo ni mengi…ila jaribu kujiwekea vipaumbele….WOTE TUMEPEWA MWAKA 2020, Kwa makusudi maalumu, tambua kusudi lako, chukua hatua kutimiza kusudi lako. Kadri unavyoishi katika kusudi lako ndipo unaongeza hamasa Zaidi ya kuishi maisha yenye furaha na kutumia muda kwa makusudi maalumu kwa umakini mkubwa.

Jedwali likionyesha mgawanyiko wa sekunde, dakika, saa, siku na Mwaka

Wote tumepewa SIKU 365, WIKI 52 na MIEZI 12…Katika kila siku tumepewa Masaa 24, hakuna kiumbe kilichopewa Zaidi ya siku, saa au wiki hata miezi Zaidi katika mzunguko wa Mwaka 2020. Hivyo ni jukumu lako kutumia muda kwa malengo uliyojiwekea, maana kila lengo litakugharimu muda na rasilimali zingine.

MWISHO, Muda mali, utumie kwa manufaa yako, maana ni mali tuliyopewa bure, ila utakavyoutumia vibaya kuna ghara kubwa unalipa, au utailipa. Ninakutakia kila la kheri katika kuishi kusudi lako na Mwaka 2020 ukawe wenye mvuto na Baraka kubwa maishani mwako.

--

--

Jeremiah Paul Wandili

| Community Development | BDSPM Consultant| YALI Alumni, Founder & Executive Director @woteinitiative Youth Leadership Advisory Board, Member #YLAB @DOTTanzania